Monday 29th April 2024
logo

SIMAMIENI VYEMA MAADILI YA UTANGAZAJI- KATIBU MTENDAJI

KATIBU Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Omar Said Ameir akiwa na Maafisa wake katika vituo vya Zanzibar Cable Television (ZCTV), Hits FM Redio na Assalaam FM Redio alipofanya ziara ya kukagua vituo vya Utangazaji Zanzibar.

WAANDISHI wa habari, wahariri na waandaaji vipindi katika vituo vya Zanzibar Cable Television (ZCTV), Hits Fm Redio na Assalaam FM Redio wametakiwa kuandika, kuhariri na kuandaa vipindi vyenye ubunifu ambavyo vitakuwa na tija katika kuelimisha jamiii.
Katibu Mtendaji wa Tume ya Utangazaji Zanzibar, Omar Said Ameir ameeleza hayo wakati alipofanya ziara katika vituo vya Utangazaji vya ZCTV na vituo vya Redio vya HITS FM na Assalaam FM Redio vilivyopo huko Mazizini, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.
“Wahariri simamieni vyema waandishi wa habari na kazi wanazowasilisha kwa kuzihariri kwa kufuata maadili ya uandishi ili kulinda amani ya nchi,” alisisitiza.
Alisema chombo cha habari ni muhimu sana katika kuijenga amani ya nchi na kinapotumiwa vibaya kinaweza kuleta athari kwa taifa hivyo alisisitiza usimamizi mzuri katika uandaaji taarifa.
Katibu Mtendaji Omar aidha amesifu juhudi zinazochukuliwa na wawekezaji binafsi katika tasnia ya Utangazaji Zanzibar, ikiwa ni pamoja na vituo vya Redio, Televisheni na Mitandao ya Kijamii kwa kuwa wanachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo la ajira kwa vijana.
Wakati huo huo amewataka wale wote wanaojishughulisha na uendeshaji wa vituo vya mitandao ya kijamii kujisajili kisheria ili kuepuka hatua za kisheria kuchukuliwa dhidi yao.
.

Other Top Story